Timu ya Coastal Union imeandaa mikakati madhubuti ya kuhakikisha inajikwamua katika nafasi ya hatari ya kucheza michezo ya mchujo (play off) kusaka nafasi ya kubaki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao
Kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu Bara, timu mbili zitakazoburuza mkia (ya 15 na 16), zitashuka moja kwa moja kwenda kucheza Ligi ya Championship msimu ujao, wakati zitakazomaliza nafasi ya 13 na 14, zitalazimika kucheza mechi za play off ili kuwania kubaki Ligi Kuu.
Ligi Kuu Bara kwa sasa ipo ukingoni zikiwa timu zote zikibakiza michezo mitano kufikia mwisho wa msimu wa 2022/23, isipokuwa Simba na Yanga tu ambazo zimebakisha mechi sita kila mmoja.
Yanga ipo kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 65 ikifuatiwa na Simba 57 huku Singida Big Stars ikifuata kwa alama zake 48 na Azam ikiwa nyuma yake kwa pointi 47.
Costal Union ipo katika nafasi ya 13 ikiwa na alama 26, ambayo ni ya kucheza michezo ya play off.
Afisa Habari wa Coastal Union, Jonathan Tito, amesema wanajipanga ipasavyo kuhakikisha wanafanikiwa kumaliza katika nafasi nzuri kwa kushinda michezo yote iliyobaki.
"Kikosi chetu kimeingia kambini kikitokea mapumziko ya wiki moja baada ya mchezo wetu wa mwisho dhidi ya Singida Big Stars ambao tulitoka sare ya bao 1-1"
"Mchezo wetu unaofuata ni dhidi ya Dodoma Jiji ambao tutacheza katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma, hivyo mwalimu anakiandaa vema kikosi chetu ili tuweze kupata matokeo mazuri," alisema Tito"
"Mchezo wetu utakuwa mgumu kutokana na nafasi tuliyopo kwa sasa, hivyo tunapaswa kujiandaa vizuri."
Michezo iliyobaki kwa Costal Union mbali ya huo dhidi ya Dodoma Jiji, ni dhidi ya Mtibwa Sugar, Ihefu, Azam FC na Simba ambao utakuwa mchezo wa mwisho utakaochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam