Singida BS yampumzisha Dario hadi msimu ujao

Joel JJ By Joel JJ β€’ 24th March 2023


Singida BS yampumzisha Dario hadi msimu ujao

Mmoja wa wachezaji waliokuwa tishio kwenye ligi kuu ya NBC mwanzoni mwa msimu ni pamoja na winga wa Singida Big Stars Dario Frederico

Dario aliuanza msimu kwa kasi kubwa akiisaidia Singida Big Stars kupata matokeo muhimu katika mechi za mwanzoni mwa msimu

Hata hivyo winga huyo raia wa Brazil baadae akakumbana na changamoto ya majeraha ya mara kwa mara hali iliyomfanya asionekane katika kikosi cha Singida BS

Dario alirejea kwao Brazil kwa ajili ya matibabu na Wanasingida hawatamuona tena katika mechi zilizosalia msimu huu

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Singida BS, nyota huyo amemaliza likizo ya mwezi mmoja liyokuwa amepewa na uongozi hata hivyo klabu imeamua kumuongezea muda wa mapumziko ili aweze kuwa imara zaidi

"Dario Frederico amemaliza likizo yake ya mwezi mmoja na ripoti ya daktari inaonesha amepona kwa zaidi ya 90%. Hata hivyo, klabu kupitia kwa ushauri wa kitaalamu wa daktari imemuongezea muda Dario ili aweze kuwa timamu kwa 100% apate na muda wa kutosha wa kupumzika"

"Kutokana na maamuzi haya, Dario atarejea rasmi wakati wa maandalizi ya ligi kuu msimu ujao wa 2023/24. Wadau na mashabiki wa Singida Big Stars watarajie kumuona Dario akiwa kwenye kiwango bora zaidi atakapoungana na timu kwenye kambi yetu ya Pre-season nchini Tunisia," ilisema taarifa ya Singida BS


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.