Kocha Msaidizi wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania, Hemed Suleiman 'Morocco' amesema wamejianda kushinda mchezo wa marudiano wa kuwania kufuzu fainali za Afcon dhidi ya Uganda Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam siku ya kesho Jumanne
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mapema leo, Morocco alisema kuwa wamewaanda wachezaji wao kimbinu na kisaikolojia kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na kuendelea kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu fainali hizo.
"Wachezaji wetu wote wapo katika hali nzuri na kila mmoja anatambua umuhimu wa ushindi, ingawa tunajua mchezo utakuwa mgumu kwa sababu Uganda watakuja kwa nguvu, lakini tumejipanga kuhakikisha tunawadhibiti na kushinda mchezo huo," alisema Morocco.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Misri Ijumaa iliyopita Tanzania iliibuka na ushindi wa bao 1-0 na kupanda mpaka nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi F baada ya kufikisha alama nne
Algeria inaongoza kundi F ikiwa na alama tisa baada ya kushinda mechi zote tatu
Mchezo huo utashuhudiwa bure na mashabiki wa soka nchini baada ya tiketi zote za mzunguuko kununuliwa na wadau mbalimbali ikiwa na sehemu ya hamasa kuhakikisha Stars inapata sapoti kubwa ya mashabiki



