Robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) inaanza kutimua vumbi wikiendi hii, ambapo Singida Big Stars (SBS) inatarajiwa kuwakaribisha Mbeya City katika mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Liti, mkoani Singida kesho Jumapili
Mchezo mwingine utapigwa Jumatatu, April 03 Azam FC wakitarajiwa kuwakaribisha wakata miwa wa Manungu, Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi
Ni mchezo wa kutoana jasho kutokana na umuhimu wa kila mmoja kutaka ushindi ili kusonga mbele hatua ya nusu fainali na hata fainali na kuchukua taji ambalo litawapa uwakilishi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Singida Big Stars ilitinga hatua hii baada ya kuwaondosha vinara wa Championship, JKT Tanzania kwa bao 1-0 mchezo uliochezwa mjini Singida. Mbeya City ilitinga hatua hii baada ya kuwaondosha Kagera Sugar kwa bao 1-0 katika mchezo wa hatua ya 16 bora uliochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.
Mechi nyingine ambazo zitahusisha klabu za Simba na Yanga zitapigwa wiki ijayo
April 07 Simba itaumana na Ihefu Fc katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Uhuru wakati April 08 mabingwa watetezi Yanga wataumana na geita Gold katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Azam Complex, Chamazi