Katika kuhakikisha timu yao inakuwa tayari kusaka ushindi kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Yanga siku ya Jumapili (April 16), baadhi ya viongozi Klabu ya Simba SC kutoka kamati mbalimbali wamehamishia shughuli zao kambini ili kuwaongezea wachezaji wao hamasa
Kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara, Yanga na Simba zilitoka sare ya bao 1-1. Na sasa Yanga kileleni mwa ligi ikiwa na alama 68 mbele ya Simba wenye alama 60
Taarifa kutoka Simba SC zimeeleza kuwa, tangu kikosi hicho kimeingia kambini huko Mbweni baadhi ya viongozi wamekuwa wakishinda huko na kutoka usiku mnene ili kuhakikisha wanawatia moyo na nguvu wachezaji wao
"Kiukweli tangu tuingie kambini kuna baadhi ya viongozi wamekuwa hawaishi mazoezini na kambini nadhani lengo ni kuendelea kutoa hamasa kwa ajili ya mechi yetu ijayo ambayo kila kiongozi anatutaka tuifunge Yanga," alisema mtoa taarifa
Kwa upande wa Meneja Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema:
"Ukubwa na umuhimu wa mchezo huu kwetu ni lazima tushikamane maana tunahitaji kuifunga Yanga. Hakuna kiongozi au Mwanasimba anayetaka kuwaona Yanga wakitangaza ubingwa dhidi yetu, hivyo tumejipanga kuvuna ushindi maana hatujawafunga muda na sasa heshima yetu pekee ni kuwapa kichapo"