Erling Haaland alifikia rekodi ya mabao 32 ya Mohammed Salah Ligi Kuu ya Uingereza huku Manchester City ikizidi kuwasogelea viongozi Arsenal baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya Leicester City Jumamosi jioni
John Stones aliwaweka mbele mabingwa hao watetezi ndani ya dakika tano za mwanzo kwa shuti la mbali likiwa bao lake la kwanza la ligi msimu huu
Mabao mawili ya Haaland katika dakika 20 zilizofuata yalimfanya afikishe jumla ya mabao 32, katika msimu wa mechi 38 wa Ligi Kuu akiifikia rekodi ya Mohamed Salah kwa Liverpool mnamo 2017/18
Haaland hakuweza kuivunja rekodi hiyo kwani alitolewa wakati wa mapumziko na Pep Guardiola kabla ya mechi ya robo fainali ya UEFA Champions League, ya mkondo wa pili dhidi ya Bayern Munich Jumatano.
Baada ya mabadiliko zaidi ya kocha huyo wa Man City, kasi ya mechi ilipungua na Leicester kurudisha bao kupitia kwa Kelechi Iheanacho dhidi ya klabu yake ya zamani na kuwapa hofu zaidi wapinzani wao.
Ushindi wa sita wa ligi mfululizo unaipa Man City pointi 70, huku kushindwa kwa timu ya Dean Smith katika mechi yake ya kwanza kuinoa Leicester kuwaacha Foxes nafasi ya 19, wakiwa na pointi 25