Uongozi wa JKT Tanzania FC umeweka wazi kwa sasa tayari malengo yao ya kutwaa ubingwa wa Ligi ya Championship msimu huu na kupanda daraja kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao yametimia kwa asilimia 90
JKT Tanzania inayonolewa na Kocha Malale Hamsini, ndio vinara wa Ligi ya Championship wakiwa na pointi 62 huku nafasi ya pili ikishikwa na Pamba ya Mwanza yenye pointi 51, kila timu imebakiza mechi tatu ili kumalizika kwa msimu huu.
Katibu wa JKT Tanzania, Kapteni Speratus Lubinga, amesema timu yao imejipanga kufanya vyema kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika michezo mitatu iliyobaki na kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara kwa heshima.
Lubinga alisema anafahamu kufanya vyema kwa timu yao kulitokana na uongozi wa kikosi cha JKT kuwa bega kwa bega na benchi la ufundi la timu hiyo na kuwahamasisha wachezaji wakati wote wanapokuwa ndani na nje ya uwanja.
"Sina mengi lakini natoa shukrani za dhati kwa uongozi mzima wa Jeshi la Kujenga Taifa likiwa chini ya Mkuu wa JKT Meja Jenerali, Rajabu Mabele, pamoja na Mkuu wa Tawi la Utawala, Brigedia Jenerali Hassan Mabena, ambao wamekuwa wakiongeza hamasa kwa wachezaji ya kupata matokeo mazuri," alisema kiongozi huyo.
Aliongeza mpaka sasa wametimiza asilimia 90 ya malengo yao kuelekea kukata tiketi ya kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu ujao.
Alitaja mechi tatu walizobakisha ni dhidi ya Kitayosce ya Tabora, Pamba, ambazo watacheza ugenini na watamaliza msimu nyumbani kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kwa kuwakaribisha Mashujaa.
"Kikosi kipo imara, lengo letu ni kuhakikisha tunaibuka na ushindi na kutwaa ubingwa wa Ligi ya Championship kwa msimu huu, tutakuwa tumetimiza maagizo ya Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa ambaye alitaka kuona kikosi kinarejea Ligi Kuu katika msimu ujao, sina shaka na wachezaji wangu, wanajituma kwa kuhakikisha timu inarudi," aliongeza.
Ametoa wito kwa wadau na mashabiki wa JKT kujitokeza kwa wingi ili kuongeza hamasa kwa wachezaji katika mechi zilizobakia