Wakati Wydad Casablanca kutoka Morocco ikiwa imewasili tayari kwa mchezo wa mkondo wa kwanza robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika, Simba iko tayari na kamili kurudia ilichokifanya mwaka 2003 kwa kuwavua taji waliokuwa mabingwa wa Afrika, Zamalek ya Misri
Simba itawakaribisha mabingwa watetezi, Wydad katika mechi itakayochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jumamosi April 22
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema baada ya miaka 20, imefika wakati Simba ikaweka rekodi nyingine ya kuwavua ubingwa Wydad kama walivyofanya mwaka 2003.
"Tuna shughuli moja tu ya kwenda kumnyoa Wydad Casablaca ili tuandike historia nyingine ya kumvua mtu ubingwa. Tunajua mechi ni ngumu, tunacheza na mtu aliyetudizi viwango vya CAF, tunacheza na mabingwa watetezi, lakini Wanasimba tukiunganisha nguvu na kushikamana, Wydad Casablaca hawana pa kutokea," alisema Ahmed
Wydad Casablanca ilitua jana mchana ikiwa na msafara wa watu zaidi ya 50, ambao ni wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na baadhi ya mashabiki.