Mkufunzi wa Simba Robertinho Oliviera amesema wamejiandaa kimbinu zaidi, kuelekea mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca.
Simba tayari imewasili salama nchini Morocco tayari kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya wenyeji wao hao itashuka dimbani Ijumaa ya Aprili 28 mwaka huu kwenye uwanja wa Mohammed V, nchini humo katika mji wa Casablanca.
Robertinho amesema kuwa maandalizi waliyoyafanya kuelekea mchezo huo wa marudiano ni mazuri na hawatakuwa wanyonge kwa sababu malengo yao ni kutaka ushindi.
Alisema ana imani kubwa na wachezaji wake kuonyesha kiwango kizuri zaidi walichokionyesha kwenye mechi ya kwanza waliyocheza uwanja wa Benjamin Mkapa na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
"Tunajua mechi dhidi ya Wydad Casablanca itakuwa ngumu sana, lakini tumejiandaa na mipango yetu ni kufikia malengo tuliyojiwekea kama timu," alisema.
"Sisi sio timu nyepesi tena watu watuheshimu tunaweza kwenda ugenini na tukafanya kitu, tunawaheshimu Wydad, lakini hatutacheza kinyonge pale Casablanca tumekuja kupigania heshima ya klabu hii kubwa," aliongeza Robertinho
Alisema wanatambua umuhimu na ugumu wa mechi hiyo na wanacheza kwa pamoja na kuwa makini na safu ya ushambuliaji ya Wydad Casablanca, mechi iliyopita walitengeneza nafasi na kushindwa kuzitumia.
Robertinho alisema wamewaona Wydad Casablanca wanapocheza nyumbani na kutakiwa kuwachunga sana kila sehemu ndani ya uwanja ili kurejea nchini wakiwa tayari wametinga nusu fainali.
Alisema anachokiangalia zaidi ni kuhakikisha wanakuwa makini katika mchezo huo ambao wanahitaji kutafuta matokeo mazuri ili kuwapeleka kucheza nusu fainali ikiwa ni mipango yao kwa sasa