Kocha Mkuu wa Simba Robertinho Oliveira ameeleza kufurahishwa na morali ya wachezaji wake kuelekea mechi ya marudiano robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya Wydad Athletic
Kesho Ijumaa, majira ya saa 3 usiku, Simba itashuka uwanja wa Mohammed V huko Morocco kuwakabili Wydad katika mchezo ambao Simba itaingia ikiwa mbele kwa ushindi wa bao 1-0 uliopatikana kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Akizungumza baada ya kikosi chake kukamilisha mazoezi yao ya kwanza tangu watue Morocco, Robertinho amesema kikosi chake kiko katika hali nzuri. Wachezaji wanajituma na kuonyesha utayari mkubwa wa kuwakabili Wydad
"Ninafurahishwa na vile wachezaji wanavyopokea maelekezo. Ari ni kubwa na kila mmoja anaonekana kuwa tayari kwa ajili ya mchezo siku ya Ijumaa. Tunafahamu tuna mechi ngumu hapa Morocco, tunaandaa mpango mzuri wa kimbinu kukabiliana na mchezo huo"
"Nimesema mara nyingi, tunahitaji kucheza kwa malengo tunapokuwa na mpira na hata pale tunapokuwa hatuna mpira. Tunao uwezo wa kupata matokeo mazuri hapa, wachezaji wetu wako tayari kuhakikisha tunafanikiwa," alisema Robertinho
Simba itakamilisha mazoezi ya mwisho leo katika uwanja wa Mohammed V tayari kwa mchezo huo ambao Simba itahitaji ushindi au matokeo yoyote ya sare ili kutinga nusu fainali