Bado dakika 90 kwa Yanga kutinga fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Marumo Gallants katika mchezo wa nusu fainali mkondo wa kwanza
Wakicheza kwa nidhamu kubwa vijana Nasreddine Nabi walihitaji dakika 30 za mwisho kuibuka na ushindi huo mnono kwa mabao ya Stephane Aziz Ki na Bernard Morrison
Aziz Ki alifunga bao la kwanza kwenye dakika ya 64 akimalizia pasi murua kutoka kwa Tuisila Kisinda
Baada ya kuingia kwa bao hilo Marumo Gallants waliokuwa bora katika kipindi cha pili, waliongeza kasi kusaka bao la kusawazisha lakini ilikuwa kama mtego kwao
Shambulizi la kushitukiza dakika za majeruhi likamshuhudia Morrison akifunga bao la pili baada ya pasi kutoka kwa Fiston Mayele
Ulikuwa mchezo mgumu lakini Yanga imefanikiwa kuondoka na ushindi muhimu ambao wataenda nao Afrika Kusini wakiwa na faida ya mabao mawili nyumbani
Ni dakika 90 tu zimebaki kwa Yanga kuweka rekodi ya kutinga fainali ya kombe la Shirikisho






