Huku ikiwa katika hatari ya kushuka daraja, Polisi Tanzania imesema itapambana kwa 'jasho na damu' kuhakikisha inavuna pointi sita katika mechi zake mbili zilizobakia za Ligi Kuu Tanzania Bara, imefahamika
Polisi Tanzania imebakisha mechi mbili zote za ugenini ambazo ni dhidi ya Simba na Azam FC, zote za Dar es Salaam.
Maafande hao wako katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara mkononi wana pointi 25, wakiwa mbele ya Ruvu Shooting yenye pointi 20 ambayo inaburuza mkia na rasmi imeshashuka daraja.
Afisa Habari wa Polisi Tanzania, Frank Lukwalo, alisema timu yao haijakata tamaa na imejipanga kuonyesha soka la burudani katika mechi zilizobakia ili malengo yao ya kupata ushindi yatimie.
Lukwalo alisema wachezaji wao watacheza kwa tahadhari kwa sababu wanahitaji kupata ushindi katika mechi zao bila kujali matokeo ya michezo mingine yatakavyokuwa.
"Tumejipanga kutumia kauli mbiu yetu ya machozi, jasho na damu, ili kuhakikisha tunavuna alama sita zitakazotuwezesha kubaki katika Ligi Kuu Bara"
"Mwalimu Zahera (Mwinyi), anaendelea na mikakati yake ya kukisuka vyema kikosi ili tupate ushindi kwenye mechi zetu mbili zilizobakia dhidi ya Simba na Azam FC"
"Mikakati bado inaenda vizuri katika mechi hizi zilizobakia tufanye vizuri, hatujakata tamaa hadi sasa na hakuna mchezaji yoyote aliyekata tamaa hadi mwisho wa ligi, hali ya kikosi ipo vizuri kuelekea michezo hiyo," alisema Lukwalo