Matola, Rweyemamu wateuliwa timu za vijana Simba

Joel JJ By Joel JJ β€’ 31st May 2023


Matola, Rweyemamu wateuliwa timu za vijana Simba

Klabu ya Simba leo imemtangaza Patrick Rweyemamu kuwa Mkuu wa Programu za Vijana wa Simba wakati Selemani Matola akitangazwa kuwa Kocha Mkuu wa timu za vijana U-17 na U-20

Mtendaji Mkuu wa Simba Imani Kajula amesema Simba imedhamiria kuimarisha timu zake za vijana akiamini huo ndio utaratibu unaotumiwa na timu zote zilizofanikiwa

"Ukichunguza timu kubwa za Afrika wana timu za vijana imara ambazo baadae wanaingia kwenye timu ya wakubwa. Leo tunatoa taarifa la kuboresha timu za vijana, la kwanza ni Mkuu wa Programu za Vijana wa Simba, Patrick Rweyemamu"

"Hakuna mtu bora kumfanya kuwa Kocha Mkuu wa timu za Vijana kama Selemani Matola. Hii inajumuisha timu za vijana za miaka 20 na miaka 17," alisema Kajula

Rweyemamu amesema hii ni hatua muhimu iliyochukuliwa na uongozi wa Simba kwani walishakuwa na utaratibu huu hapo nyuma na walifanikiwa

"Mpira hauwezi kuendelea bila kuwa na uwekezaji kwa vijana. Tulishawahi kufanya hii kazi na matunda yake yanajulikana. Kuanzia 2008 hadi 2015 tumetoa wachezaji takribani 250. Hakuna timu za Ligi Kuu hadi madaraja ya chini hayajawahi kukosa wachezaji ambao wamepita kwenye timu ya vijana ya Simba"

"Tunatafuta wachezaji wenye vipaji, wenye uwezo, tunatengeneza ajira na tunapunguza mchakato wa usajili sababu kutafuta kitu ambacho hujawekeza kina gharama yake"

"Kuna kizazi kinapotea kwenye mpira hivyo lazima tuandaje kizazi kipya ambacho kitasaidia Simba na Taifa kwa ujumla," alisema Rweyemamu

Nae Kocha Selemani Matola amewapongeza viongozi wa Simba kwa kurejesha utaratibu wa timu za vijana ambao walikuwa nao zamani na walifanikiwa

"Kwanza tupongeze Bodi na uongozi kwa kuona hili, kwetu sisi sio jambo geni. Tulishafanya na tulifanikiwa sana. Naamini sasa tutazalisha vitu vizuri zaidi ikiwezekana zaidi ya ile ya mwanzoni. Sitawaangusha wapenzi wa Simba, tafanya wanachotaka mimi nifanye kwenye Youth Development," alisema Matola


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.