Jana Yanga ilicheza mechi ya kuhitimisha kilele cha wiki ya Mwananchi dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini
Mchezo huo wa Kimataifa wa kirafiki ulipigwa uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 1 usiku Yanga ikiibuka na ushindi wa bao 1-0
Mfungaji wa bao pekee la Yanga alikuwa ni Kennedy Musonda akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Max Nzengeli
Furaha ya mashabiki wa Yanga ni kuwashuhudia nyota wao wapya wakiwa katika kiwango bora
Kulikuwa na maneno mengi katika dirisha hili la usajili kila timu ikitamba kufanya usajili mzuri, nyota waliosajiliwa na Yanga wamedhihirisha ubora wao katika siku ya kwanza kazini
Nickson Kibabage, Jonas Mkude, Max, Skudu Makudubela, Yao Yao, Gift Fred wote wakipata nafasi ya kucheza dakika 45
Mkude aliwapagawisha mashabiki wa Yanga kwa uwezo wake wa kupiga pasi ndefu wakati Max anaweza kuwa shujaa mpya katika kikosi cha Yanga kutokana na umahiri wake anapokuwa na mpira mguuni
Kibabage alionyesha umahiri pale timu inaposhambulia akishirikiana vyema na Skudu
Kwa hakika ulikuwa mchezo mzuri ambao umewapa picha mashabiki wa Yanga nini watarajie kutoka kwa timu yao



