Kiungo mshambuliaji wa Yanga Max Mpia Nzengeli amesema ametua kwa mabingwa hao wa Tanzania Bara kufanya kazi moja tu, kuwapa furaha mashabiki kwa kuhakikisha timu inapata ushindi
Juzi katika mchezo wa wiki ya Mwananchi dhidi ya Kaizer Chiefs, Nzengeli alitoa 'pasi ya upendo' kwa Kennedy Musonda aliyefunga bao pakee la Yanga katika mchezo huo ambao Wananchi waliibuka na ushindi wa bao 1-0
Baada ya mchezo huo Nzengeli alikuwa gumzo wengi wakifurahishwa na uwezo mkubwa alioonyesha katika dakika 45 alizocheza
"Nimekuja hapa kufanya kazi, sina kawaida ya kuahidi jambo lolote lakini nawaambia mashabiki waendelee kutuunga mkono sisi wachezaji. Tutaendelea kupambana ili kuisaidia timu ipate ushindi," alisema Nzengeli
Katika mchezo huo, Nzengeli ambaye Yanga ilimsajili kutoka AS Maniema Union kama winga, kocha Miguel Gamondi alimtumia nafasi ya kiungo mshambuliaji (10)
Nzengeli, Mudathir Yahya na Jonas Mkude walitengeneza utatu wa aina yake katika eneo la kiungo wakitawala na kusukuma mashambulizi kwa haraka
Nzengeli ataipa faida Yanga msimu ujao kwani anaweza kutumika katika nafasi yoyote kwenye eneo la ushambuliaji




