Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Simba Ahmed Ally amewataka mashabiki waendelee kununua tiketi kuelekea SIMBA DAY ambayo itafanyika August 06 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Ahmed amewahakikishia Wanasimba kuwa Tamasha hilo litafanyika uwanja wa Benjamin Mkapa kama lilivyopangwa, maboresho ya uwanja huo hayaingiliani na ratiba ya Tamasha hilo kubwa zaidi la michezo nchini
"Baada jana kutangazwa ukarabati wa Uwanja wa Benjamini Mkapa, wengi wamekuwa na hofu juu mustakabali wa Tamasha letu la Simba Day"
"Taarifa rasmi ni kwamba hakuna mabadiliko ya Uwanja, Simba Day yetu itafanyika pale pale nyumbani kwetu Benjamini Mkapa"
"Muhimu mashabiki endeleeni kununua tiketi," aliandika Ahmed katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii
Katika hatua nyingine, Ahmed amesema bado mpinzani ambaye atacheza na Simba kwenye SIMBA DAY ni Mabingwa wa Ligi Kuu ya Zambia, Power Dynamo licha ya uwezekano wa Simba kukutana na Dynamo kwenye raundi ya kwanza ligi ya mabingwa barani Afrika
"Mpaka sasa bado hakuna mabadiliko, mpinzani tutakaecheza nae kwenye SIMBA DAY ni Power Dynamo. Tunafahamu upo uwezekano wa kukutana nao kwenye ligi ya mabingwa, kwa upande mwingine hii inafikirisha kidogo kwa sababu tunaweza tukacheza nao mara tatu"
"Lakini Simba ina viongozi makini ambao wanajua vyema kazi yao, kama wataona kuna ulazima wa kubadili mpinzani kwa muktadha wa kiufundi basi watatuambia ingawa kwa muda uliobaki sioni kama hilo litatokea"