Kiungo mshambuliaji wa Yanga Skudu Makudubela amepona majeraha akiwa miongoni mwa wachezaji wanaojifua kwa ajili ya mchezo wa kuwania tiketi ya kutinga hatua ya makundi ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya El Merrikh
Kikosi cha Yanga kitasafiri Rwanda kuikabili El Merrikh katika mchezo wa mkondo wa kwanza utakaofanyika uwanja wa Pele, Septemba 16
Skudu alipata majeraha katika mchezo wa nusu fainali Ngao ya Jamii dhidi ya Azam Fc, akicheza kwa dakika saba tu katika mchezo ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0
Baadae hakuonekana tena uwanjani akiuguza majeraha hayo lakini sasa amepona na kurejea rasmi kikosini
Mashabiki wa Yanga tayari wameona ubora wa nyota wote waliosajiliwa isipokuwa Skudu tu, ambaye pengine wanaweza kumshuhudia nchini Rwanda
Kabla ya kupata majeraha Skudu alikuwa miongoni mwa wachezaji wa kikosi cha kwanza cha kocha Miguel Gamondi
Alitumika kwa dakika 45 katika mchezo wa Kimataifa wa kirafiki dhidi ya Kaizer Chiefs na pia kucheza mechi kadhaa za kirafiki Avic Town
Baada ya kuyaona makali ya Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua 'profesa', bila shaka ni zamu ya Skudu kuonyesha alichowaletea Wananchi