Wekundu wa Msimbazi Simba Sc leo wanaanza kampeni ya kusaka tiketi ya kutinga makundi katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika
Simba iliyoanzia raundi ya kwanza katika michuano hiyo, leo inachuana na Power Dynamos katika mchezo ambao utapigwa uwanja wa Levy Mwanawasa huko Zambia
Huu ni mchezo muhimu kwa Simba kushinda ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya makundi na kuendeleza rekodi yao nzuri katika michuano hiyo
Kwa miaka mitatu mfululizo Simba imeingia hatua ya makundi ya mashindano ya CAF na pia ikifanikiwa kutinga robo fainali
Msimu huu Simba imejiwekea malengo ya kuvuka robo fainali lakini kabla ya kuwaza hatua hizo za juu ni lazima kuvuka hatua za chini kwanza
Kikosi cha kocha Robertinho Oliveira kiko Zambia tangu siku ya Alhamisi jana wachezaji wakipata nafasi ya kufanya mazoezi yao ya mwisho katika uwanja wa Levy Mwanawasa
Jana Robertinho aliwaambia wanahabari kuwa wanatarajia mchezo huo utakuwa mgumu, lakini wamejipanga vyema ili kupata matokeo mazuri
Mchezo utapigwa saa 9 Alasiri kwa saa za Zambia wakati Tanzania itakuwa saa 10 jioni