Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema kikosi chake kimekamilisha maandalizi kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya Namungo Fc ambao utapigwa kesho Jumatano katika uwanja wa Azam Complex
Licha ya uchovu na baadhi ya wachezaji kuwa majeruhi, Gamondi amesema anaimani na wachezaji wote, yeyote anaweza kumtumia kwenye mchezo huo na timu ikapata matokeo mazuri
"Jana Tulianza maandalizi kuelekea mchezo wetu na Namungo, tuna baadhi ya wachezaji wana uchovu na wengine wana majeraha lakini nina imani na wachezaji waliopo benchi kwa sababu najua wanaweza kutupa matokeo chanya," alisema Gamondi
Aidha Kocha huyo raia wa Argentina amebainisha kuwa siri ya mwendelezo mzuri wa matokeo ya kikosi chake inatokana na kazi nzuri wanayofanya kwa pamoja kati ya benchi la ufundi na wachezaji
Amesema falsafa yake ni kujenga timu imara ambayo kila mmoja anashiriki na hakuna utegemezi wa mchezaji mmoja mmoja
"Nimeona wengi wakiongelea ubora wa baadhi ya wachezaji lakini kwangu mimi dira yangu sio mchezaji mmoja mmoja bali timu nzima. Ndio maana utagundua timu yetu tunacheza mchezo mzuri, na mchezaji yoyote anaweza kufunga"
"Nimejenga mazingira ya kuwa na timu iliyo na uwiano mzuri kwa kila idara, tazama tumefunga magoli mengi lakini vile vile tumeruhusu goli moja tu katika michezo saba tena bao la penati ambalo ilikuwa kosa letu"
"Sasa ili uwe na uwiano na namna hiyo lazima ujenge timu inayotegemeana na sio timu inayomtegemea mtu fulani kwenye idara fulani"
"Jambo ambalo nimezingatia kwanza ni wachezaji kuheshimiana wenyewe kwa wenyewe, pili wachezaji kuheshimu falsafa zangu, huwezi kuwa kocha mzuri kama wachezaji hawakuheshimu. Kimsingi matokeo chanya ya sasa ni kutokana na jitihada za wachezaji na benchi la ufundi," alisema Gamondi
Kesho Jumatano majira ya saa 1 usiku Yanga itashuka uwanja wa Azam Complex kumenyana na Namnungo Fc katika mchezo ambao matokeo ya ushindi kwa Yanga yatawarudisha kileleni mwa msimamo wa ligi



