Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema kikosi chake kitakuwa tayari kuikabili Azam Fc kwenye mchezo wa ligi kuu utakaopigwa Jumapili, Oktoba 22 katika uwanja wa Azam Complex
Mchezo huo umerudishwa nyuma baada ya mabadiliko ya ratiba yaliyofanywa na Bodi ya Ligi, awali ulipangwa kupigwa Oktoba 25
Gamondi amesema wamekaa muda mrefu pasipo kucheza mechi hivyo mchezo huo kurudishwa nyuma ni jambo jema
"Nimefurahishwa na mabadiliko ya ratiba, kwani awali nilikuwa naumiza kichwa namna ya kupata mechi ya kirafiki ili kuwajenga kimwili na kiushindani wachezaji ambao wamekaa nje ya uwanja kwa muda bila kucheza," alisema kocha huyo raia wa Argentina
Aidha Gamondi amesema anaamini wachezaji walio kwenye majukumu ya timu za Taifa watarejea kwa wakati tayari kwa mchezo huo
"Djigui Diarra, Stephane Aziz Ki na Khalid Aucho wanacheza mechi za mwisho za kirafiki wakitumikia timu za taifa, Oktoba 18 nimewaambia warudi siku inayofuata ili kujiandaa na mchezo huo kwani ni mchezo mgumu na wenye ushindani mkubwa"
Nyota wa Yanga waliokuwa timu ya Taifa ya Tanzania wanatarajia kurejea nchini leo baada ya kukamilisha ratiba ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Sudan uliopigwa Saudi Arabia jana na kumalizika kwa sare ya bao 1-1