Yanga imerudi kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya NBC baada ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Azam Fc katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Moja ya mechi bora kushuhudiwa kwenye ligi kuu msimu huu, mechi ikiamuliwa na mchezaji mkubwa Stephane Aziz Ki aliyefunga hat-trik
Aziz Ki alifunga bao lake la kwanza kwenye mchezo huo katika dakika ya nane baada ya kuwatoka walinzi wa Azam Fc na kuweka mpira kimiani
Azam Fc walirejea mchezoni kwenye dakika ya 18 kupitia kwa Gibril Sillah ambaye shuti lake la mguu wa kushoto lilimshinda mlinda lango wa Yanga Djigui Diarra
Hata hivyo picha za marudio zinaonyesha Sillah alipkea mpira akiwa kwenye eneo la kuotea kabla ya kupiga shuti lililojaa upande wa kushoto wa Diarra
Mpaka mapumziko timu hizo zilikuwa zimetoshana nguvu kwa sare ya bao 1-1
Yanga waliwaheshimu sana Azam Fc kwenye kipindi cha kwanza lakini vijana wa Gamondi walirejea wakiwa na moto katika kipindi cha pili
Hata hivyo ni Azam Fc waliofunga bao la pili dakika ya 63 kupitia mkwaju wa penati wa Prince Dube baada ya Sillah kuangushwa kwenye eneo la hatari na nahodha Mwamnyeto
Yanga iliongeza kasi ya mashambulizi na Aziz Ki kufunga mabao mawili ya haraka haraka kwenye dakika za 69 na 72
Alifunga bao la pili kupitia mpira wa adhabu kabla ya kuongeza la tatu baada ya pasi kutoka kwa Aucho
Ulikuwa mchezo mgumu ambao kwa hakika wachezaji wa Yanga walivuja jasho jingi kupata ushindi huo
Yanga imepanda kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 15






