Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) imewahakikishia mashabiki wote watakaoingia uwanja wa Benjamin Mkapa kushuhudia mchezo wa dabi ya Kariakoo kati ya Simba dhidi ya Yanga siku ya Jumapili, usalama utakuwa wa kutosha
Aidha, TPLB imewataka mashabiki wanaokwenda na silaha uwanjani kuzisalimisha kituo cha polisi kilicho karibu na uwanja huo na baada ya mechi watafuata silaha zao
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Habari wa TPLB, Karim Boimanda wakati akizungumzia maandalizi kuelekea mchezo huo utakaopigwa Jumapili, Novemba 05 saa 11 jioni
"Kuna mashabiki wanaingia na silaha uwanjani, hivyo kwa yeyote anayemiliki silaha na anatembea nayo basi siku hiyo atalazimika kuacha kituo cha Polisi maana hataruhusiwa kuingia nayo"
"Mashabiki watakaguliwa, maana kule ndani usalama utakuwepo wa kutosha kutoka Jeshi la Polisi," alisema Boimanda
Boimanda amesema mageti siku hiyo yatafunguliwa kuanzia saa 4:00 asubuhi hivyo amewataka mashabiki kukata tiketi mapema ili kuepuka usufumbufu na wale watakaopewa mialiko maalumu kuhakikisha hawagawi mialiko yao kwa mtu mwingine.



