Uongozi wa klabu ya Simba umewaomba radhi mashabiki baada ya kupoteza mchezo wa watani wa jadi dhidi ya Yanga uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa jana
Aidha Simba imewashukuru mashabiki kwa kujitokeza kwa wingi katika mchezo huo ambao ulimalizika kwa Simba waliokuwa wenyeji kufungwa mabao 5-1
Meneja wa Habari na Mawasiliano Ahmed Ally amesema ni maumivu makali kila Mwanasimba anapitia baada ya kipigo hicho
Maumivu hayo yatadumu kwa muda mrefu kwani matokeo hayo tayari yameingia katika vitabu vya kumbukumbu
Hata hivyo jambo la msingi ni kuwa mchezo huo umepita, kila sehemu yenye mapungufu imeonekana libaki kuwa jukumu la uongozi, benchi la ufundi na wachezaji kusahihisha
Haupaswi kuwa wakati wa kulaumiana kwani kuna mechi nyingine ya Ligi Kuu inafuata siku chache zijazo dhidi ya Namungo Fc (Alhamisi) na huu ni mchezo ambao Simba inahitaji kushinda
"Kwenye Mkutano wa Wanahabari nilisema, Hii ni mechi ambayo matokeo yake hua yanaacha furaha ya kudumu au huacha maumivu ya kudumu kwenye mioyo ya mashabiki wake"
"Bahati mbaya ni sisi ndo tunabaki na maumivu ya kudumu Kila Mwana Simba anawaza sababu tafauti tofauti iliyosababisha tupoteze mchezo wa jana"
"Iko namna sahihi ya kujua sababu hizo nayo ni utulivu.Tuwape viongozi, benchi la ufundi na wachezaji wetu utulivu wa kujitathmini kwa maslahi ya mechi zijazo"
"November 9 kuna mchezo dhidi ya Namungo hivyo ni vema tukajikita zaidi kuangalia tunachukuaje alama tatu hizo baada ya kupoteza jana," alisema Ahmed



