Timu ya Mashujaa yenye maskani yake Kigoma jana imepoteza mechi ya nne mfululizo katika Ligi Kuu baada ya kufungwa mabao 3-1 na Singida Big Stars katika Uwanja wao wa nyumbani Lake Tanganyika
Mashujaa ilianza kupoteza pointi ugenini Oktoba 3 kwa JKT Tanzania ikifungwa bao 1-0, ikacheza tena Oktoba 25 dhidi ya Coastal Union na kufungwa 2-0 na ikarudi nyumbani Kigoma Novemba 1 kuikabili Azam FC ambapo Mashujaa ilifungwa mabao 3-0
Baada ya vipigo hivyo, mashujaa imeporomoka mpaka nafasi ya 10 ikiwa na pointi 8 (katika mechi 8 ilizocheza ikiwa na kiporo cha Simba) huku Singida BS ikipanda nafasi ya 7 na pointi 12 katika mechi 9
Mashujaa iliyopanda ligi kuu msimu uliopita, ilianza ligi kibabe ikishinda mechi mbili mfululizo nyumbani na kukaa juu ya msimamo wa ligi kabla ya kulazimishwa sare katika mchezo wa tatu
Mambo yaliwaharibikia walipoanza kusafiri kucheza nje ya Kigoma na hata waliporejea tena nyumbani wakaendelea kupigwa