Kocha Mkuu wa Simba Abdelhak Benchikha ana kibarua kizito cha kuwavusha Wekundu wa Msimbazi robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika
Simba inakabiliwa na dakika 180 ngumu dhidi ya Wydad Athletic ya Morocco katika mechi mbili ambazo zitaamua hatma ya wababe hao wa soka katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati
Msimu uliopita Simba ilianza vibaya mechi mbili za hatua ya makundi ikipoteza zote lakini ilifanikiwa kufuzu robo fainali kwa kushinda mechi tatu
Msimu huu pia haijaanza vyema kwani imetoka sare mechi mbili za mwanzo na kukusanya alama mbili tu sasa ikishika nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi B
Inakwenda kumenyana na Wydad iliyo katika mazingira magumu zaidi, ikiwa imepoteza mechi zote mbili za mwanzo
Mchezo wa kwanza utapigwa Disemba 09 huko Morocco na mchezo wa pili kupigwa Disemba 20 jijini Dar es salaam
Simba inahitaji angalau alama nne kutoka katika mechi hizi mbili ili kuweka hai matumaini ya kutinga robo fainali
Benchikha hakuwa na mwanzo mbaya katika majukumu yake na Simba licha ya timu yake kulazimishwa suluhu ya bila kufungana dhidi ya Jwaneng Galaxy siku ya Jumamosi
Simba ilionyesha mabadiliko makubwa katika mchezo huo ambao ilikuwa ugenini, ilitawala na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga
Akiwa na uzoefu mkubwa katika mashindano ya CAF, hakuna shaka chini ya Benchikha, Simba inaweza kuvuka salama katika mechi dhidi ya Wydad