Mtibwa Sugar itakuwa ugenini Jumamosi dhidi ya Yanga ambao wanarudi kwenye ligi baada ya kukosekana kwa muda kutokana na kubanwa na ratiba ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katwila aliyejiunga na timu hiyo Oktoba, mwaka huu akitokea Ihefu FC, ameiongoza katika mechi sita na kushinda moja, ameliambia amesema kuwa wanaendelea na maandalizi kuhakikisha kikosi kinarudi kwenye ushindani bila kujali wanakutana na timu gani.
"Tutaingia kwa kuwaheshimu Yanga Jumamosi na siyo kuwaogopa tunacheza na timu yenye wachezaji 11 kama sisi na changamoto tunayoipitia ni kipindi cha mpito timu nyingi huwa zinapitia nyakati ngumu kama hizi matokeo haya hayanifurahishi, nimeandaa programu nyingine za mazoezi na kuwapa wachezaji muda zaidi wa mazoezi wa kuongeza viwango vyao," alisema
Kocha huyo alisema anataka kuiona Mtibwa Sugar ikiendelea kushiriki Ligi Kuu na kupanda juu katika msimamo. Mtibwa Sugar inaburuza mkia ikiwa na pointi tano baada ya kushuka dimbani mara 12.
Kocha huyo aliiongoza Mtibwa Sugar kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Geita Gold kabla ya kufungwa bao 1-0 na KMC kisha kupoteza 2-1 ilipocheza na JKT Tanzania na kukubali kipigo cha mabao 5-0 dhidi ya Azam FC huku ikikubali kufungwa mabao 2-1 na Tabora United kisha kuchapwa bao 1-0 na Namungo
Wakati yuko Ihefu Fc, Katwila aliwaongoza walima mpunga hao kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Yanga na sasa anakutana tena na Wananchi akiwa na Mtibwa Sugar