Kocha Mkuu wa Simba Abdelhak Benchikha anaanza 'project' ya kukisuka upya kikosi cha Simba katika dirisha dogo la usajili kazi ambayo atakwenda kuikamilisha katika usajili wa dirisha kubwa mwezi Juni/Julai
Imeelezwa wachezaji ambao atawasajili kwenye dirisha dogo ni wale ambao wanahitaji haraka ili kumaliza changamoto katika baadhi ya maeneo lakini kiuhalisia ni kuwa Simba itahitaji maboresho makubwa zaidi baadae
Eneo la kiungo mkabaji limekuwa wimbo wa Simba, licha ya usajili wa Fabrice Ngoma ambaye hata Benchikha alimwagia sifa kuwa antimiza vyema majukumu yake uwanjani, kilio cha kiungo mkabaji hakijamalizika
Simba inahusishwa kumuwania kiungo wa Kimataifa wa Chad Eric Mbangossoum mwenye umri wa miaka 23 anayeitumikia klabu ya Union Touarga ya Morocco, nchi ambayo Benchikha amewahi kufanya kazi katika klabu za Mouloudia d'Oujda, Difaa El Jadida, Raja Casablanca na RS Berkane kabla ya kujiunga na USM Alger
Hata hivyo kumpata Mbangossoum, Simba itahitaji kuvunja mkataba wake wenye thamani ya karibu Milioni 600. Huyu ni mchezaji ambaye Simba inaweza kumtumia hata kwenye michuano ya ligi ya mabingwa kama itafanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali