Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Yanga Ali Kamwe amewaalika mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi uwanja wa Azam Complex katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa Jumamosi
Kamwe amesema baada ya kushuhudia mazoezi ya Yanga kwa siku tatu yakifanyika katika uwanja wa Avic Town, amejiridhisha wachezaji wako tayari na wanautaka kwelikweli mchezo huo
Aidha Kamwe amesema malengo ya Yanga ni kufunga mwaka 2023 kibabe kwa kushinda mechi zote za ligi watakazocheza mwezi huu Disemba
"Nawaambia mashabiki wetu waje kwa wingi uwanja wa Azam Complex siku ya Jumamosi, tumewaandalia burudani ya soka itakayoambatana na magoli mengi"
"Mwananchi hakikisha Jumamosi unamaliza shughuli zako mapema ili uwahi Azam Complex kwani uwanja huu tunafahamu haubebi mashabiki wengi"
"Ari ya timu ni kubwa, wachezaji wako tayari nadhani Jumamosi mashabiki watashuhudia burudani nyingine ya aina yake kutoka kwa timu yao," alitamba Kamwe
Yanga imekuwa na rekodi nzuri katika mechi walizocheza dhidi ya Mtibwa Sugar katika misimu ya karibuni
Yanga imeshinda mechi sita zilizopita dhidi ya Mtibwa Sugar pasipo kuruhusu bao
Ikicheza katika uwanja wa Azam Complex msimu huu, Yanga imeshinda mechi zote zikiwemo za Ligi Kuu na hatua ya awali Ligi ya Mabingwa