Alama zote tatu zimebaki Msimbazi baada ya Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa uwanja wa Uhuru
Ulikuwa ushindi wa kwanza kwa Kocha Abdelhak Benchikha ambaye leo ameiongoza Simba katika mchezo wake wa kwanza kwenye ligi
Simba iliuanza mchezo taratibu hata hivyo ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Sadio Ntibazonkiza kupitia mkwaju wa penati baada ya Ntibazonkiza mwenyewe kufanyiwa madhambi ndanii ya eneo la hatari
Simba iliongeza kasi ya mashambulizi kwenye kipindi cha pili ilikuwa ni suala la mabao mangapi Simba yatafungwa
Baada ya kosakosa nyingi Sadio Kanoute aliyetumika kama kiungo wa ushambuliaji leo akafunga bao la pili kwenye dakika ya 74 akiunganisha krosi ya Mohammed Hussein
Nahodha John Bocco yawezekana mashabiki wamepoteza imani kwake lakini yeye ameendelea kuifanya kazi yake vyema kila anapopewa nafasi akifunga bao la tatu kwenye dakika za lala salama
Bocco amefunga mabao mawili msimu huu yote akiyafunga akitokea benchi
Ni alama tatu muhimu kwa Simba ambazo zinawapandisha mpaka nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 22
Aidha ni ushindi ambao utaweka saikolojia ya wachezaji sawa kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Wydad utakaopigwa Jumanne katika uwanja wa Benjamin Mkapa



