Mabao mawili aliyofunga Stephane Aziz Ki katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mtibwa Sugar, yamemfanya kiungo mshambuliaji huyo kuweka rekodi ya aina yake msimu huu
Juzi Aziz Ki aliisaidia Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa uwanja wa Azam Complex, Chamazi
Nyota huyo wa Kimataifa kutoka Burkina Faso, amefikisha mabao 9 baada ya mechi 10 msimu huu akiongoza orodha ya wafungaji bora
Ki ameivunja rekodi ya Fiston Mayele ya msimu uliopita ambapo baada ya mechi 10 alikuwa amefunga mabao saba na kutoa pasi mbili za mabao. Ki amefunga mabao 9 pia akitoa pasi mbili za mabao
Aziz Ki amehitaji mechi 10 tu kufikia rekodi yake ya mabao 9 aliyofunga msimu uliopita
Gamondi amtabiria ufungaji bora
Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema nyota huyo kama ataendelea kuwa katika ubora alionao sasa, ni wazi ataibuka mfungaji bora msimu huu
"Mwanzoni mwa msimu nilimwambia Aziz Ki, ana kipaji na uwezo wake wa kupiga mashuti ni kitu tofauti, akitumia vyema kipaji na maarifa yake, atafunga mabao mengi"
"Amefunga mabao mawili (dhidi ya Mtibwa Sugar) lakini utaona nafasi nyingine alikosa, angeweza kufunga hata mabao manne"
"Kama ataendelea kucheza hivi, nadhani ana nafasi kubwa ya kuibuka mfungaji bora," alisema Gamondi
Wakati baadhi ya wachambuzi wakiiona Yanga ina changamoto kwenye safu ya ushambuliaji lakini ndio timu yenye kinara wa mabao mpaka sasa Aziz Ki ambaye takwimu zake ni bora kuliko hata takwimu za Mayele baada ya mechi 10 za kwanza za msimu