Kocha Mkuu wa Simba Abdelhak Benchikha ameendelea kukiandaa kikosi chake kuelekea mchezo muhimu wa ligi ya mabingwa dhidi ya Wydad ambao utapigwa kesho Jumanne katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Simba inahitaji kushinda mchezo huu ili kuweka hai matumaini ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo. Hivyo huu ni mchezo ambao dakika zake 90 zitaamua hatma ya Simba katika michuano hiyo ambayo malengo yaliyowekwa msimu huu ni angalau kucheza nusu fainali
Jana Simba ilikamilisha mazoezi yake ya mwisho katika uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo baada ya mazoezi hayo Benchikha aliwahakikishia Wanamsimbazi kuwa kikosi chake kiko tayari na watafurahi baada ya dakika 90 za mchezo huo
Benchikha alisema hakuna timu isiyofungika huku akiwataka mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao katika mchezo huo muhimu
"Hakuna timu isiyofungika, tuondoe mawazo hasi kichwani kwetu tutaingia uwanjani tukiwa kifua mbele na lengo likiwa ni kushinda. Tunawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kuipa nguvu timu yao naamini baada ya mechi tutafurahi kwa pamoja," alisema



