Kamati ya mashindano ya Kombe la Mapin-duzi kwa mwaka 2023 imetoa ratiba yote ya mashindano hayo, huku wababe wa soka la Tanzania Yanga na Simba wakifunga na kufungua mwaka 2023 na 2024 mtawalia
Kombe la Mapinduzi litaanza Desemba 28, 2023 kwenye Uwanja wa Amaan uliofanyiwa ukarabati mkubwa na kuwa wa kisasa
Mabingwa watetezi Mlandege watafungua mashindano hayo kwa kucheza na URA SC ya Uganda saa 10:15 jioni na baadaye Azam FC, mabingwa mara tano wa Kombe la Mapinduzi watakuwa wageni wa Chipukizi kutoka kisiwani Pemba, mchezo ambao utachezwa kuanzia saa 2:15 usiku
Yanga SC itashuka dimbani Desemba 31 kuwakaribisha Bandari ya Kenya saa 2:15 usiku, wakati Singida Fountain Gate watacheza na APR ya Rwanda Januari 1, 2024
Simba SC, mabingwa mara nne wa Mapinduzi Cup watashuka dimbani kuvaana na Jamhuri kutoka Pemba Januari 1, 2024 saa 2:15 usiku
Michezo yote hiyo itachezwa kwenye Uwanja wa Amaan na mchezo pekee ambao unatarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Gombani kule kisiwani Pemba ni wa nusu fainali ya kwanza ambayo utamkutanisha mshindi wa robo fainali ya kwanza dhidi ya yule wa robo fainali ya pili utakaochezwa Januari 10, 2024




