Timu ya Azam imeendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya jana kuendeleza wimbi la ushindi wakiichapa Kagera Sugar mabao 4-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba
Mabao ya Azam yalifungwa na Feisal Salum 'Fei Toto' dakika ya '9, Prince Dube dakika ya 11, Pascal Msindo dakika ya 45 na Alassane Diao dakika ya 84 na kuifanya timu hiyo kufikisha jumla ya pointi 31 katika michezo 13 iliyocheza hadi sasa
Pointi hizo 31 ilizonazo Azam zinaifanya kuendelea kujikita kileleni na kuiacha Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa taji hilo ikiwa na 27 ingawa imecheza michezo 10 ambayo ni mitatu pungufu ya vinara hao kwa sasa wa Ligi Kuu Bara msimu huu
Baada ya kufunga bao katika mchezo huo, Fei Toto amefikisha jumla ya mabao manane ya Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi hicho msimu huu akipitwa moja tu na kinara wa Yanga, Stephane Aziz KI anayeongoza akiwa amefunga tisa
Ushindi wa Azam unaifanya timu hiyo kufikisha jumla ya michezo sita mfululizo ya Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza tangu mara ya mwisho ilipofungwa mabao 3-1, dhidi ya Namungo Oktoba 27, mwaka huu kwenye uwanja wake wa Azam Complex, Chamazi



