Licha ya kuwepo kwa tetesi za mshambuliaji Moses Phiri kuandika barua ya kuomba kuvunja mkataba wake kutokana na kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza, hatma yake imebaki mikononi mwa kocha Abdelhak Benchikha
Phiri mmoja wa wachezaji ambao Wanamsimbazi walikuwa na matumaini makubwa kwake, imekuwa si rahisi kwake kupata nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza tangu wakati Simba ikinolewa na Robertinho Oliveira
Nyota huyo kutoka Zambia ambaye msimu huu amefunga mabao matatu, pia amekosa nafasi katika mechi za mwanzo za kocha wa sasa, Benchikha
Hata hivyo taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Simba imebainisha kuwa, hatma yake itategemea na ripoti ya Benchikha ambayo wataifanyia kazi katika dirisha hili dogo la usajili ambalo litafungwa Januari 15 2024
Inafahamika Phiri anahusishwa na Yanga hivyo hata ikitokea Simba itaamua kuachana nae, lazima makubaliano hayo yatahakikisha haendi upande wa pili katika dirisha hili
Nyota huyo alisajiliwa na Simba msimu uliopita kutoka Zanaco baada ya mabosi wa Msimbazi kuwazidi Yanga waliokuwa wakimpigia hesabu na kumfuata hadi Zambia ili kumshawishi
Phiri alikuwa na wakati mzuri chini ya kocha Juma Mgunda akiibeba Simba Ligi ya Mabingwa msimu uliopita na kwenye ligi kabla ya kuumia na kukaa nje kwa muda mrefu, hadi alipoingia Robertinho.



