Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dr. Ali Hassan Mwinyi amesema serikali yake ipo katika mpango wa ujenzi wa viwanja vingine vya mpira huku akiahidi michuano ya Afcon 2027 itafanyika katika uwanja huo mpya
Rais Mwinyi aliyasema hayo jana katika uzinduzi wa uwanja wa Amaan baada ya ukarabati mkubwa. Uzinduzi huo ulikwenda sambamba na mchezo wa kirafiki kati ya Zanzibar Heroes dhidi ya Kilimanjaro Stars uliomalizika kwa suluhu ya bila kufungana
Aidha, Rais Dk.Mwinyi ameeleza kuwa Serikali imelenga kujenga miundombinu ya michezo kila wilaya kwa viwanja vipya vya kisasa

Vilevile Rais Dk.Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Ujerumani kupitia shirika la maendeleo GIZ imefunga mkataba wa makubaliano kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vitano vya michezo midogomidogo ikiwemo mpira wa kikapu, mpira wa wavu , mpira wa mikono na mpira wa pete
Viwanja hivyo vinatarajiwa kujengwa Kangani Wilaya ya Mkoani, Mchangamdogo Wilaya ya Wete, Tumbatu na Mkokotoni Wilaya ya Kaskazini A na Haile Selasie Wilaya ya Mjini pamoja na viwanja vitatu vya Tennis Chakechake, Chuo kikuu cha SUZA Kampasi ya Nkurumah na Skuli ya Regeza Mwendo katika Wilaya ya Magharibi B
Halikadhalika Serikali ya Zanzibar imefanikiwa kuwapeleka vijana katika nchi mbalimbali ikiwemo Uturuki na Afrika Kusini kwa lengo la kuendelezwa na baadae kucheza soka la kulipwa.
Rais Dk.Mwinyi amewahimiza wananchi kushiriki Tamasha la kila mwaka la mazoezi linalofanyika tarehe Mosi ya mwaka mpya.