Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi ameeleza kufurahishwa na usajili wa kiungo mshambuali Augustine Okrah akibainisha kuwa mchezaji huyo atakuwa na mchango katika kikosi chake
Hata hivyo Gamondi amesisitiza ni lazima apambane kwenye kiwanja cha mazoezi ili kujihakikishia nafasi ya kucheza
Okrah alisajiliwa na Yanga katika dirisha dogo akitokea klabu ya Bechem United ya kwao Ghana
Ni mmoja wa wachezaji watatu waliosajiliwa kwenye dirisha dogo wengine wakiwa Shekhan Khamis na Joseph Guede
"Nimemuona Okrah ni mchezaji mzuri naamini ataongeza kitu katika eneo letu la ushambuliaji. Hata hivyo ni lazima apambane katika kiwanja cha mazoezi kwani utaratibu wetu hapa tunatoa nafasi kwa mchezaji anayefanya vizuri mazoezini kwani kile tunachokifanya mazoezini ndicho tunakifanya kwenye mechi," alisema Gamondi
Nae Okrah amesema anatambua amejiunga katika timu bora yenye wachezaji mahiri hivyo atahakikisha anatimiza vyema majukumu yake ili awe msaada kwa timu
"Natambua ubora wa kila mchezaji wa Yanga hususan maeneo ninayocheza, hilo linanifanya kuungana nao na kufanya vyema kwa ajili ya manufaa ya timu pia inanipa ari ya kupambana zaidi ili kupata nafasi kikosini"
"Mimi sio mgeni hapa Tanzania, nimewahi kucheza Simba na sasa nimerudi nikiwa na Yanga nadhani tutakuwa na safu bora zaidi ya ushambuliaji," alisema