Licha ya kuwepo taarifa za kufutwa kazi kwa Kocha Mkuu wa kikosi cha timu ya Taifa Tanzania ‘Taifa Stars’ Adel Amrouche, lakini Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro ameweka wazi kuwa kocha huyo yuko sana katika kikosi cha Stars
Waziri huyo amesema Serikali iko pamoja na kocha huyo hata pale adhabu yake ya kufungiwa mechi nane na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) itakapomalizika
Dkt. Ndumbaro amesema kuwa kocha huyo raia wa Algeria amefanya makubwa na ndiye aliyeifikisha timu kwenye michuano ya AFCON inayoendelea huko nchini Ivory Coast, hivyo watakuwa nae katika changamoto anazopitia na hawatasitisha mkataba wake
"Bado sisi kama Serikali ambao ndiyo walipa mshahara ukiadhibiwa sio muda wa kumzodoa, tupo naye kwenye kipindi hiki kigumu anachopitia"
"Bado tuna imani nae, yeye ndiye aliyetufikisha hapa sehemu ya kufuzu. Mwalimu huyu ndiye ametengeneza timu hii, tupo na mwalimu, hatujasitisha mkataba, ameadhibiwa na CAF, hajaadhibiwa na serikali wala TFF"
"Sisi katika kipindi hiki kigumu ambacho mwalimu ana kipitia tuko nae na tutaendelea kuwa nae, kumpa sapoti yote ambayo inahitajika, ili yeye apite kwenye kipindi hiki kigumu kwa salama kabisa" alisema Dkt. Ndumbaro
Baada ya kocha huyo kufungiwa, kikosi hicho kwa sasa kipo chini ya makocha wa muda Hemed Suleiman na Juma Mgunda