Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amewashukuru Wananchi wa Bukoba kwa mapokezi makubwa waliyoipatia timu yao leo ilipowasili kutoka Dar es salaam kupitia Mwanza
Mamia ya mashabiki wa Yanga walijitokeza kwa wingi uwanja wa ndege wa Bukoba kuwapokea wachezaji wao walioambatana na benchi la ufundi na viongozi kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar utakaopigwa kesho Ijumaa
Gamondi amesema mapokezi hayo yamewapa hamasa kubwa akiahidi kuwapa furaha kwa kuibuka na ushindi dhidi ya Kagera Sugar
"Nawashukuru sana mashabiki waliojitokeza kutupokea hapa, walichofanya leo ni jambo la kipekee. Kiukweli tumegushwa na kile tulichoshuhudia hapa ni hamasa kubwa kwetu kuelekea mchezo wa kesho," alisema Gamondi
Akizungumzia maandalizi ya mchezo Gamondi alisema wachezaji wote wako tayari kwa mchezo huo na mkakati wao ni kuvuna alama tatu na kuwapa furaha mashabiki wao
Yanga itakamilisha mazoezi ya mwisho leo katika uwanja wa Kaitaba ambapo uongozi wa Yanga umetoa ofa kwa mashabiki watakaojiandikisha kuwa Wanachama kuingia uwanjani kushuhudia mazoezi hayo