Ihefu Fc meendelea kutoa vichapo kwa wapinzani Ligi Kuu baada ya usajili mkubwa walioufanya kwenye dirisha dogo kwa kuwaleta mastaa kibao akiwemo mshambuliaji, Elvis Rupia na kiungo Marouf Tchakei ambao wameendelea kuibeba katika michezo ya Ligi Kuu
Baada ya kuipa Ihefu ushindi 3-2 kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar, nyota hao leo wameifungia mabao muhimu timu hiyo na kuiwezesha kuondoka na ushindi wa mabao 2-1 ugenini mbele ya Geita Gold kwenye Uwanja wa Nyankumbu, mjini Geita, ukiwa ni ushindi wa pili mfululizo
Rupia aliitanguliza timu yake mapema katika dakika ya tano kwa kichwa akiunganisha krosi ya Marouf Tchakei, kabla ya Tchakei naye kuweka chuma cha pili katika dakika ya 12 akimalizia pasi ya Hernest Malonga na kwenda mapumziko wikiwa kifua mbele kwa mabao 2-0
Baada ya kufunga leo katika mchezo huo ambao ulianza saa 8:00 mchana, Tchakei anafikisha bao lake la saba kwenye Ligi Kuu, huku Rupia akifikisha bao la tatu
Geita Gold imekubali kichapo cha kwanza nyumbani kwenye Uwanja wa Nyankumbu tangu Septemba 30, 2023 ilipofungwa mabao 2-1 na KMC, ambapo baada ya hapo ilicheza mechi tano dimbani hapo bila kupoteza ikishinda tatu na sare mbili
Ihefu imelipa kisasi cha kufungwa bao 1-0 katika mzunguko wa kwanza mchezo uliopigwa Agosti 15, 2023 kwenye Uwanja wa Highland Estates, Mbeya.