Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, amesema mechi bado zipo nyingi ambazo zinaweza kuipatia Simba ubingwa wa Tanzania Bara, lakini amesisitiza ni lazima wachezaji waongeze umakini na kutumia vyema nafasi nyingi wanazotengeneza katika kila mechi
Matola amesema hawapaswi kukata tamaa kwa kuangalia matokeo ya timu nyingine kwa sababu ligi ni kama mbio ndefu, anayechanga karata zake vizuri mwishoni mwa kumalizika ndiyo mshindi na si yule anayeongoza kwa muda mrefu
"Siwezi kusema eti ubingwa basi kwa sababu kuna timu inafanya vizuri, sisi bado tupo kwenye mbio hizo na tuna imani tunaweza kuupata"
"Siku zote ligi ni kama mbio ndefu, mwanariadha anaweza kuongoza kwa muda mrefu, akawa mbele kilometa nyingi, lakini zikibaki mita kadhaa watu wanapindua kibao, hii ni raundi ya 20, lakini sisi Simba tumecheza mechi 17, hivyo michezo mingi imebaki , huwezi kututoa kwenye ubingwa," alisema Matola.
Matola pia amezungumzia changamoto ya ratiba ambayo inawanyima muda wa kufanya maboresho zaidi ya kimbinu kwa sababu ya kucheza kila baada ya siku mbili
"Ratiba ni changamoto pia, wakati mwingine tunakosa muda wa kufanya baadhi ya maandalizi kwa kuwa kila baada ya siku mbili tunacheza mechi"
"Tunaishia kufanya mazoezi ya 'recovery' kuwaandaa wachezaji na mechi inayofuata lakini yote kwa yote tutaendelea kupambana, timu inawachezaji bora na wengine wana uzoefu mkubwa naamini watatusaidia kufikia malengo yetu"
Leo saa 2:15 usiku Simba itashuka dimba la Azam Complex kumenyana na Singida FG ukiwa mchezo wa raundi ya 18 NBC PL