Mshambuliaji Clement Mzize, amesema hatasikiliza 'kelele' za mashabiki na badala yake ataendelea kufuata maelekezo anayopewa na kocha wake, Miguel Gamondi, ili kuisaidia timu Yanga kupata matokeo mazuri katika mechi zake
Juzi Mzize aliiongoza Yanga kutinga robo fainali ya kombe la Shirikisho la CRDB akifunga bao la pili katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji
Nyota huyo ambaye bado ni 'kinda', amesema anafurahi kuona Gamondi anampa nafasi ya kucheza na anamwamini hali inayomtengenezea kujiamini na kufanya vizuri
Mzize alisema licha ya kutofanya vizuri katika michezo miwili iliyopita jambo lililozalisha 'maneno' juu yake, aliongeza bado hatayapa nafasi anapokuwa uwanjani.
"Mara nyingi Kocha Miguel ananiambia natakiwa kufuata maelekezo yake anayonipa mazoezi na kuhamishia uwanjani, ananiamini na nisipaniki, nisitoke mchezoni kwa sababu ya kutofanya vizuri katika mechi mbili zilizopita"
"Nitajituma na kupambana kila ninapopata nafasi ya kucheza ili kuhakikisha ninafunga na kutafuta tuzo ya ufungaji bora wa michuano hiyo (Kombe la FA), sitasikiliza maneno ya nje," alisema Mzize
Mzize ndio kinara wa mabao katika michuano ya FA akifunga mabao matano