Serikali ina mpango wa kuunda timu tatu imara za soka za Taifa kulingana na umri ambazo zitashiriki mashindano ya Afcon 2027 na mengine ambayo nchi itashiriki
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma amesema hayo leo Jumatatu Aprili 30, 2024 alipojibu maswali ya nyongeza ya Mbunge wa Jimbo la Magomeni, Mwanakhamis Kassim Said (CCM)
Mbunge huyo amehoji Serikali ina mkakati gani wa kuandaa timu ya Taifa ili ishindane kwenye michuano ya Afcon. Pia amehoji ni kwa jinsi gani wasanii watashirikishwa kwenye fainali za Afcon 2027
Naibu Waziri, Mwinjuma amesema Serikali imeandaa mkakati wa kuandaa timu si tu kwa ajili ya Afcon 2027, bali kwa mashindano mengine ambayo Tanzania itashiriki na zitagharamiwa na Serikali kwa asilimia 100
Amesema moja ya mkakati ni kutengeneza timu tatu za Taifa zitakazopishana umri ya kwanza itakuwa ni ya vijana chini ya miaka 17, itakayotokana na wanafunzi wa michezo ya Umiseta ya kila mwaka
"Tukishawapata wachezaji hawa tutawaweka kwenye shule moja ambayo tumeshaiteua na watasimamiwa na walimu magwiji. Itapata mechi za mazoezi ya kutosha za ndani na nje. Kila mwaka wachezaji hao tutakuwa tunawapeleka kwenye akademi zenye mafanikio nje ya nchi ili kuendeleza vipaji tayari kulitumikia Taifa," amesema
Mwinjuma amesema timu ya pili, itakuwa inayoundwa na vijana wenye umri wa chini ya miaka 23, ambao wanacheza ligi mbalimbali ndani na nje ya nchi na watakuwa wakikutana wakati wakiwa kwenye mapumziko ya timu zao
Mwinjuma amesema Tanzania kwa kushirikiana na nchi za Kenya na Uganda itakuwa mwenyeji wa mashindano ya Afcon 2027
"Ili kuhakikisha timu ya Taifa inafanya vizuri katika mashindano hayo, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo ujenzi wa viwanja vya mpira katika majiji ya Dodoma na Arusha," amesema
Amesema pia utafanyika ukarabati wa Viwanja vya Benjamin Mkapa na Uhuru, na kuwatafuta na kuwaleta nchini wachezaji wenye asili ya Tanzania wanaoishi na kucheza nje ya nchi ili kuchezea timu ya Taifa.