Licha ya timu yake kupoteza mchezo wa ufunguzi michuano ya Mpumalanga Premier's International Cup dhidi ya Augsburg, Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema ameridhishwa na kiwango klichoonyeshwa na vijana wake
Yanga ilifungwa mabao 2-1 katika mchezo ambao ilionyesha ubora mkubwa katika kipindi cha pili
Gamondi amesema ilikuwa heshima kubwa kwa Yanga kucheza na Augsburg inayoshiriki ligi kuu ya Ujerumani na anaamini kile walichokionyesha katika mchezo huo kimemfurahisha kila mpenda soka barani Afrika
"Hatukucheza vizuri sana kwenye kipindi cha kwanza kulikuwa makosa ya hapa na pale lakini hii ni kawaida hasa ukizingatia tulifanya mazoezi kwa wiki moja tu kabla ya mchezo huu ambao pia ni wa kwanza kwetu katika pre-season"
"Lakini pia tusisahau tumecheza dhidi ya Augsburg, timu ya ligi kuu ya Ujerumani (Bundesliga) hivyo isingekuwa rahisi kwa wachezaji wetu"
"Kipindi cha pili tulikuwa bora zaidi, tulifunga bao na pia tulikuwa na nafasi dakika za mwisho tungeweza kusawazisha"
"Matokeo hayakuwa muhimu sana kwetu katika mchezo huu. Nimefurahishwa na vile wachezaji wangu walivyopambana na kufanya kile tulichohitaji kutoka kwao," alisema Gamondi
Yanga itacheza mechi nyingine mbili hapo Afrika Kusini kabla ya kurejea Tanzania tayari kwa wiki ya Mwananchi



