Dabi ya Kariakoo presha juu

Joel JJ By Joel JJ β€’ 7th August 2024


Dabi ya Kariakoo presha juu

Homa ya pambano la watani wa jadi, Simba na Yanga limeanza kuwapata wanachama na mashabiki wa timu zote mbili, ambapo pamoja na kila upande kutamba, lakini kumekuwa na angalizo kutokana na kile kilichoonekana kwenye mechi za matamasha yao

Timu hizo kubwa na kongwe zinazobeba taswira ya soka la Tanzania, zitavaana kesho saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam katika mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii

Wanachama na mashabiki wa Yanga wameendelea kutamba baada ya kuona kikosi chao kiko kwenye kiwango kile kile cha msimu uliopita, lakini kikiongezewa nguvu na wachezaji mastaa wanaolijua vyema soka la Bongo, Clatous Chama, Duke Abuya, Prince Dube na Jean Baleke, hivyo wamekuwa na uhakika kuwa wataendeleza ubabe wao kwa kuifunga Simba kama walivyofanya msimu uliopita, walipoifunga mara mbili kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara

Kwa upande wa wanachama na mashabiki wa Simba nao wameonekana kuwa na matumaini mapya, hasa baada ya kufanya usajili mkubwa wa wachezaji kutoka Ivory Coast, Zambia, Nigeria, Guinea, Burkina Faso na sehemu mbalimbali

Wachezaji kama Joshua Mutale, Debora Fernandes Mavambo, Jean Charles Ahoua, Augustine Okejepha, Awesu Awesu, Valentin Nouma na wengineo wameanza kuwapa kiburi mashabiki wa Simba ambao wamesema wanaweza kupata ushindi, lakini hata kama watapoteza mechi hiyo, haitokuwa kizembe kama walivyochapwa mabao 5-1 msimu uliopita

Wengi wameridhishwa na kiwango cha wachezaji wao, ingawa wanadai bado hawajazoeana na hicho pekee ndicho kinachowapa wasiwasi kwenye dabi hiyo, wengine wakisema baada ya mechi tatu tu za Ligi Kuu, hakuna timu inayoweza kuigusa tena, ikiwamo Yanga

Kocha Mkuu wa Simba, Msauzi, Fadlu Davids, amesema hivi sasa anawaandaa wachezaji wake kisaikolojia kwa ajili ya mechi hiyo. Alisema wachezaji wake ingawa mwenyewe anasema hawajaiva kwa asilimia 100 kama anavyotaka, na hii inatokana na muda kuwa mfupi kwani anaendelea kuwatengeneza, lakini wataifanya kazi kubwa kesho

"Mchezo utakuwa mzuri na mgumu, lakini nimewaandaa wachezaji wangu kisaikolojia kwenda kucheza, wakituliza akili na kufuata maelekezo, haina shaka ya kuibuka na ushindi," alisema

Simba inakwenda kucheza mechi hiyo ikiwa ndiyo mshindi wa Ngao ya Jamii iliyopita ilipolitwaa Agosti 23, mwaka jana, Uwanja wa Mkwakwani, ilipoichapa Yanga mabao 3-1 kwa mikwaju ya penalti

IPP Media


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.