Klabu ya Tabora United, imesema baada ya kufungwa mabao 3-0 dhidi ya Simba Jumapili iliyopita, Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam, sasa hasira zao wanazielekeza kwa Namungo katika mechi inayofuata
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Christina Mwagala, alisema wamekubali kuwa wamepoteza mechi kihalali dhidi ya Simba kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ugeni wa wachezaji wengi kwenye kikosi, lakini mchezo huo umewapa mazoezi tosha ya kujua uzito wa mechi za Ligi Kuu
"Tumekubali tumefungwa, lakini tumefunga na timu kubwa ya Simba, kwa hiyo nadhani mechi inayofuata tutapata ushindi kwa sababu hatuchezi tena na mnyama, bali Namungo"
"Mechi iliyopita imetupa mwelekeo na mazoezi tosha ya kujua uzito na mzani wa Ligi Kuu, nadhani sasa wachezaji watakuwa wanaelewa nini wanatakiwa kufanya baada ya mchezo huo," alisema
Mwagala alisema sababu kubwa ya kupoteza mechi hiyo ilikuwa ya kwanza, halafu inacheza na timu kubwa, huku ikiwa na wachezaji wengi wapya
"Tumesajili wachezaji 28 msimu huu, lakini kati ya hao, ni sita tu waliokuwa msimu uliopita, kwa hiyo utaona kuwa 22 wote ni wapya, unakwenda kucheza na timu kama Simba, labda kama tungecheza na timu nyingine, hilo tumemaliza nadhani mechi inayofuata tutawaonesha mashabiki wa soka kuwa Tabora United si timu ya mchezo kama wanavyofikiria," alisema
Kocha Mkuu wa timu hiyo Mkenya, Francis Kimanzi, ameendelea na mazoezi ya kukiunganisha kikosi hicho ambacho kilionekana kukosa muunganiko katika mchezo dhidi ya Simba
Tabora United ipo jijini Dar es Salaam, ikijiandaa na safari ya kwenda mkoani Lindi kucheza mechi ya raundi ya pili ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo, Jumapili ijayo, Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa