Wakati Yanga ikitarajiwa kukamilisha mechi ya pili hatua ya awali ligi ya mabingwa dhidi ya Vital'o siku ya Jumamosi, kocha mkuu wa mabingwa hao wa Tanzania Bara Miguel Gamondi ameanza kuipigia hesabu mechi ya raundi ya kwanza kwani kikosi chake kina asilimia kubwa ya kuiondoa Vital'o
Yanga iko mbele kwa mabao 4-0 ushindi wa ugenini waliopata katika mechi ya kwanza dhidi ya Vital'o. Ni muujiza pekee ambao wanahitaji Vital'o kupindua matokeo dimba la Mkapa wakihitaji kushinda mabao 5-0 ili kusonga mbele
Baada ya CBE kuruhusiwa na CAF kutumia uwanja wao wa nyumbani, kama timu hiyo itaitoa SC Villa, watakutana na Yanga katika hatua inayofuata ambapo mechi ya kwanza Yanga itaanzia ugenini na kumalizia nyumbani
Jumamosi CBE na SC Villa zitachuana katika mchezo wa marudiano utakaopigwa Adis Ababa huku CBE wakiwa mbele kwa mabao 2-1 ushindi waliopata nchini Uganda
Gamondi anatarajiwa kutuma mtaalam kutoka benchi lake la ufundi ili kwenda kushuhudia mchezo huo na kuwasoma wapinzani wake hao
Wakati SC Villa wakirejea katika michuano ya Kimataifa baada ya kupotea kwa miaka mingi, CBE ni mara yao ya kwanza kushiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuchukua ubingwa wa kwao kwa mara ya kwanza tangu ianzishwe 1982.
Timu hiyo imeshiriki mara mbili mashindano ya Afrika ambapo mara mbili ikicheza Kombe la Shirikisho Afrika na kutolewa hatua ya mtoano miaka ya 2005 na 2010 kabla ya msimu huu kuja kutanua historia yao kwa kucheza ligi ya mabingwa
Gamondi amekuwa na utaratibu wa kuwasoma wapinzani wake kabla ya kukutana nao na mara nyingi huenda mwenyewe uwanjani kushuhudia mechi zao
Lakini mechi za mkondo wa pili kati ya Yanga dhidi ya Vital'o na CBE dhidi ya SC Villa zote zitapigwa Jumamosi