Baba mzazi wa mchezaji Israel Mwenda amesema kijana wake yuko tayari kurejea kuitumikia Singida Black Stars kama klabu hiyo itatimiza masharti ya mkataba na kulipa fedha ambazo hawakukamilisha
Juzi Singida BS ilitangaza kumtaka Mwenda aripoti kambini au la afuate taratibu za kuvunja mkataba alioingia na timu hiyo ambapo klabu ilimtaka alipe Tsh Milioni 500
Hata hivyo Mwenda akaweka msimamo kuwa Singida BS hawakufuata makubaliano na ameanza mchakato wa kuvunja mkataba wa miaka miwili ambayo alisaini akitokea klabu ya Simba
Baba mzazi wa mchezaji huyo, Mzee Patrick Mwenda amesema kijana wake ameridhia kurejea kambini kama atamaliziwa fedha anazodai
"Wakitulipa leo, kesho kijana ataenda Singida. Maana sisi hatuna tatizo na timu, shida ya Tanzania uswahili ni mwingi. Sisi hicho hatuwezi kukikubali lazima kijana alipwe fedha yote halafu aende."
"Kijana alipaswa kulipwa milioni 340 kama signing on fee ni tofauti na mishahara yake ya kawaida. Signing on fee hii imegawanywa, kwamba malipo ya awali atalipwa milioni 200 na msimu wa pili atalipwa milioni 70 na msimu wa 3 milioni 70"
"Lakini taarifa ya klabu ya Singida ilisema milioni 200 tu. Maana watanzania wengi walikuwa wameshaamini kwamba kama kijana ameshalipwa milioni 140, hiyo 60 angemaliziwa baadae," alisema Mwenda
Katika milioni 200 ambazo Mwenda alipaswa kulipwa katika msimu wa kwanza, alipokea Milioni 140 tu hivyo anadai Tsh Milioni 60
Singida BS imethibitisha fedha hiyo italipwa lakini kwa kuzingatia makubaliano ya kimkataba, kampuni inayomsimamia mchezaji huyo ndio iliyochukua jukumu la kulipa kwa makubaliano ya kulipwa fedha hizo na Singida BS baadae