Licha ya ushindi wa bao 1-0 ambao Yanga walipata ugenini dhidi ya CBE SA katika mchezo wa mkondo wa kwanza kuwania tiketi ya kufuzu hatua ya makundi ligi ya mabingwa barani Afrika, Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema bado hawajafuzu hatua ya makundi hivyo wanahitaji kushinda mchezo wa marudiano
Katika makaratasi, CBE SA wanaonekana kama mpinzani mwepesi hasa baada ya kupoteza mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa Ethiopia. Gamondi hawachukulii katika wepesi huo
"Mimi naheshimu kila mpinzani ninaekutana nae katika michuano hii. Tangu mwanzo wakati tunakwenda Ethiopia nilisema hatutakuwa na mchezo mwepesi na hicho ndicho kilichotokea licha ya ushindi tuliopata"
"Tuna faida ya ushindi wa ugenini lakini haina maana tayari tumefuzu, tunapaswa kupambana katika mchezo wa pili tuweze kupata ushindi na kujihakikishia nafasi hiyo"
"CBE ni timu nzuri, tulipocheza nao mwanzo hatukuwa tukiwafahamu vyema lakini sasa tunawajua, mchezo wa pili utakuwa tofauti na tutacheza mbele mashabiki wetu ambao naamini watakuja kwa wingi kutuunga mkono"
"Licha ya kushinda, sote hatukufurahia kile kilichotokea Ethiopia, ilitakiwa kushinda kwa kiwango kikubwa lakini mambo haya yanatokea kwenye soka, ninachofurahia kila mchezaji anajutia"
"Tumefanya mazoezi ya kutosha ya kufunga mabao, naweza kusema kila kilichofanywa na washambuliaji na wachezaji wa nafasi zingine kimenivutia sana naamini tutakwenda kuwa na dakika 90 nzuri nyumbani," alisema
Uwanja wa New Amaan Complex unaochukua takribani mashabiki 15,000 uko tayari kwa mchezo huo utakaopigwa saa 2:30 usiku
Meneja wa Yanga Walter Harrison amesema wameamua kupeleka burudani ya michuano ya CAF kwa mashabiki wao wa Zanzibar ambao kama Watanzania wanastahili kupata burudani hiyo
"Zanzibar ni sehemu ya Tanzania na tuna mashabiki wengi sana hakuna mtu mwenye shaka na hilo, tulifanya tathmini ya kina na tukaona ni sehemu sahihi ya kwenda kucheza mchezo wetu wa raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika ambao Mungu akijaalia tutaingia kwenye hatua ya makundi," alisema