Kutokana na timu yao kuwa na matokeo ya kusuasua katika Ligi Kuu Tanzania Bara, uongozi wa Pamba Jiji FC, umewataka mashabiki na wanachama wa timu hiyo kuwa watulivu kwa sababu muda bado upo wa kufanyia kazi mapungufu ya kikosi chao
Pamba Jiji ina pointi nne kibindoni baada ya kushuka dimbani mara tano katika ligi hiyo
Mwenyekiti wa Pamba Jiji, Biku Kotecha, amesema mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara ni ngumu na wachezaji wao wamekuwa wakipambana kusaka matokeo chanya na wanachokipata ni kutokana na kucheza kwa juhudi
Kotecha alisema wanaendelea kurekebisha mapungufu na anaamini mechi zinazofuata watapata ushindi kwa sababu wachezaji wao wameanza kuzoea 'joto' la Ligi Kuu Tanzania Bara
"Tunawaomba mashabiki wetu wasikate tamaa, muda bado upo, hii ni Ligi Kuu, ushindani wake ni mkubwa zaidi, lakini hata ukiangalia msimamo utaona timu zimepishana pointi chache," alisema Kotecha
Pamba Jiji ambayo huu ni msimu wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu katika kipindi cha miaka 23, tangu iliposhuka daraja mwaka 2001, itarusha tena karata yake dimbani kwenye mwendelezo wa ligi hiyo, Septemba 28, mwaka huu, kwa kuwavaa wenyeji wao, Coastal Union ya jijini Tanga, Uwanja wa KMC uliopo Mwenge, Dar es Salaam



