Ni Simba au Yanga kwa Mkapa leo

Joel JJ By Joel JJ β€’ 19th October 2024


Ni Simba au Yanga kwa Mkapa leo

Unaweza kusema leo ni siku kubwa kwa wapenzi na mashabiki wa soka Tanzania pale watani wa jadi Simba na Yanga watakapochuana katika mchezo wa ligi kuu ya NBC utakaopigwa kuanzia saa 11 jioni

Unapozungumzia mechi kubwa zaidi ya mpira wa miguu Tanzania, basi so nyingine, ni hii Kariakoo Derby inayozikutanisha timu zenye upinzani wa kihistoria

Pamoja na kuwa matokeo ya mchezo wa leo hayawezi kuamua hatma kuelekea ubingwa wa ligi kuu msimu huu, lakini timu itakayoibuka na ushindi leo itajiweka juu kwenye ushinda baina ya timu hizo msimu huu

Simba iko nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi ikiwa na alama 13 wakati Yanga iko nafasi ya tano ikiwa na alama 12 pia ikiwa na mchezo mmoja wa kiporo

Yanga inakwenda katika mchezo huo ikiwa na rekodi ya kibabe dhidi ya watani zao, ikiwa imeshinda mechi tatu mfululizo zilizokutanisha timu hizo katika mashindano yote

Msimu uliopita Wananchi waliibuka kidedea katika mechi zote mbili za ligi dhidi ya watani zao wakishinda 5-1 na 2-1 na pia kushinda 1-0 mwezi August katika nusu fainali ya Ngao ya Jamii

Ni wazi leo Simba itakwenda dimba la Mkapa ikiwa na dhamira moja tu, kumaliza uteja na kurudisha ari yao katika kuwania taji la ligi kuu msimu huu

Vijana wa kocha Fadlu Davids wameanza vyema msimu wakishinda mechi nne za ligi na sare moja

Lakini bila shaka leo watahitaji kuwa katika ubora wao ili kuweza kuondoka na alama zote tatu dhidi ya Yanga iliyojipambanua kuwa timu bora kwa sasa Tanzania

Mchezo utapigwa saa 11 jioni


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.